hata wakiacha muziki hawafi njaa

Dada Mkuu’ wa Bongo Fleva, Judith Wambura 'Lady Jay Dee'.
Lucy Mgina
KATIKA maisha siku zote tunashauriana kwamba tusitegemee chanzo kimoja cha fedha. Kama wewe ni muajiriwa basi unatakiwa kuwa na vyanzo vingine vya kujiingizia kipato ili usipate tabu pindi ajira yako inapokoma. Kwa Tanzania asilimia kubwa ya wasanii na hata watu wa kawaida wamekuwa wakijisahau kuhusiana na ishu hii.
Staa wa Bongo fleva  Nasibu Abdul 'Diamond Platinumz'.
Wengi wao wakiona wametoka na wimbo ‘uka-hit’ basi huona kama wamefika na kuanza kufanya matumizi ya fedha hovyo jambo ambalo baadaye hujutia na kujikuta wakiwa ombaomba kwenye baa na mitoko mingine mbalimbali.
Lakini wapo ambao wanajielewa na kujijenga zaidi pindi wanapopata mtaji kwa kuanzisha biashara nje ya fani yao, sasa wafuatao ni baadhi ya wasanii ambao wao hata wakisema waache muziki leo hawawezi kufa na njaa kwa urahisi kama unavyodhani;
Prof Jay
Hivi karibuni Mungu akipenda ataanza kuitwa Mheshimiwa Joseph Haule kwani anagombea Ubunge Jimbo la Mikumi mkoani Morogoro kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Ana saluni ya kunyoa na nyumba kubwa yenye studio ndani yake.
Mkongwe huyo hawezi kuadhirika hata kama akiacha muziki au dili zake za siasa ‘zikibuma’.
Mzee Yusuf
Jamaa anafanya Muziki wa Taarab. Lakini nje ya fani ‘anajielewa’ kwani anamiliki malori mawili aina ya Scania ambayo yanayafanya kazi kwenye Kampuni yake ya Uuzaji na Usambazaji wa Vifaa vya Ujenzi huko Chanika pia ana biashara nyingine za maduka ya nguo. Hata leo akiacha muziki, wala hawezi kufa njaa kwani ameshajiwekea mazingira mazuri nje ya fani hiyo.
 Ally Mshamu ‘Jaffarai’.
Jaffarai
“Ndugu zangu msinitafute…Nipo bize” nadhani umekikumbuka kiitikio hicho cha kwenye Wimbo wa Nipo Bize ya msanii wa Bongo Fleva kutoka Kundi la Wateule, Ally Mshamu ‘Jaffarai’, mshkaji anamiliki ‘car wash’ yake iliyopo Mikocheni ambayo imekuwa ikijaza mastaa wenzake ambao wamekuwa wakimuunga mkono kwa kwenda kuosha magari yao pamoja na watu wengine wa kawaida.
Jamaa yupo kimya kwa muda mrefu kidogo na biashara yake ya kuosha magari inambeba kiaina.
Nikki wa Pili
Ana akili kijana! Jina lake alilopewa na wazazi wake ni Nickson Simon. Kijana huyu ana Shahada ya Uzamili katika Maendeleo na Uongozi, aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2013 na sasa anasomea Shahada ya Uzamivu (PhD) chuoni hapo hivyo kwake hata akisema aupige pembeni muziki wala haimpi shida kwani anaweza kupata kazi fasta. Tayari baadhi ya watu wameanza kumtumia kwenye mambo ya kijamii, hiyo inaweza kumbeba na kumtangaza atakapomaliza shule ikawa si tatizo katika kusaka ajira.
Lady Jaydee
‘Dada Mkuu’ wa Bongo Fleva, Judith Wambura. Anajua kazi yake ipasavyo na wala hatetereki na siku zote kazi zake zimekuwa za kiwango kikubwa.
Ukimtoa nje ya fani hiyo, msanii huyu anapiga kazi hatari licha ya kudai kuwa anakutana na changamoto mbalimbali kubwa ambazo kama angekuwa mwanamke mwingine angekata tamaa mapema.
Anamiliki ardhi, nyumba mbalimbali hapa Dar ambazo amezipangisha na nyingine anakaa mwenyewe lakini ameripotiwa kuwa na daladala ambazo anazifanyia biashara pia ndiye msanii pekee anayemiliki gari kali aina ya Range Rover Evoque.
Diamond Platnumz
Ndiye msanii aliye juu kwa sasa huku akifanya juhudi kubwa kuupeleka muziki wa Tanzania kwingineko Afrika na hata nje ya bara hili. Kijana huyu mwenye miaka 25 tayari anamiliki kampuni ya mavazi inayotumia Lebo ya Wasafi Classic, pia amewekeza zaidi kwenye ardhi na biashara nyingine mbalimbali.Tayari amejenga mjengo wake wa maana na anaishi na mpenzi wake, Zarinah Hassan ‘Zari’ ambaye amezaa naye mtoto mmoja anayeitwa Latifah.
Hata akisema leo aache muziki, itakuwa ngumu sana kwake kuwa choka mbaya kutokana na namna alivyojiweka vizuri kwenye mambo ya fedha.
Ambwene Yesaya 'AY'.
AY
Jina lake halisi ni Ambwene Yesaya ambaye alizaliwa mkoani Mtwara miaka 34 iliyopita. Mshkaji ukikutana naye katika mishe zake yupo simpo tu lakini kwenye masuala ya kimaendeleo yupo mstari wa mbele sana.
Jamaa anamiliki Kampuni ya Unity Entertainment inayotengeneza vipindi maarufu vya Mkasi na Siasa za Siasa ambavyo vinarushwa kupitia runinga ya EATV, usisahau ana maduka ya nguo na biashara nyingine kubwa tu mjini. Anaweza akapumzika au akastaafu kufanya muziki lakini akaishi kifalme tu, kwani mkwanja kwake haukatiki kiwepesi hivyo.

0 Comment "hata wakiacha muziki hawafi njaa"

Post a Comment

Thank you for your comments